Wawakilishi kutoka nchi 25 kujadili mbegu za asili
2023-08-14 11:06:23| cri

Zaidi ya wadau 100 kutoka mataifa 25 barani Afrika, Ulaya na Marekani watakutana jijini Dar es Salaam kwa siku tatu ili kujadili mbegu za asili, ambazo kwa kiasi kikubwa zinachangia usalama wa chakula katika bara la Afrika. Mratibu wa Taifa wa Muungano wa  Bioanuwai wa Tanzania (TABIO), Abdallah Mkindi alifahamisha kuwa mkutano huo utaanza Agosti 14 hadi 16, akibainisha kuwa washiriki wataangalia hatima ya mbegu za asili, ambazo hazipewi kipaumbele katika sera na sheria. Alisisitiza kuwa utafiti unaonesha kuwa mbegu za asili ni salama na ni za uhakika kwa chakula.

Alisema mkutano huo umeandaliwa kwa pamoja na Muungano wa Udhibiti wa Chakula wa Afrika (AFSA), TABIO na SwissAid. Mkindi alizitaja nchi zinazoshiriki kuwa ni Tanzania, Kenya, Uganda, Ethiopia, Senegal, Burkina Faso, Ivory Coast, Hispania, Norway, Zambia, Zimbabwe na Australia.

Nyingine ni pamoja na Togo, Mali, Benin, Chad, Tunisia, Niger, Afrika Kusini, Botswana, Malawi, Misri, Rwanda, DR Congo, na Gabon.