Museveni akataa shuruti la Benki ya Dunia juu ya sheria ya ushoga
2023-08-14 11:06:58| cri

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema nchi yake inaweza kuendelea bila mikopo ya Benki ya Dunia, ambayo imetangaza kusitisha ufadhili baada ya sheria ya kupinga ushoga ya nchi hiyo.

Badala yake, Museveni alisema Benki hiyo inatumia ufadhili wake wa miradi kuzilazimisha nchi za Afrika kukanyaga utamaduni wao, jambo ambalo alisema hatalifanya. Hivyo amewaeleza Waganda kwamba Uganda itaendelea tu kwa mkopo au bila mkopo. Amesema ni bahati mbaya kwamba Benki ya Dunia na wahusika wengine wanathubutu kutaka kuwalazimisha kuacha imani, utamaduni, kanuni na uhuru wao kwa kutumia pesa, akisistiza kuwa kwa hivyo watakuwa wanadharau sana Waafrika.

Benki ya Dunia ilisitisha ufadhili wowote wa siku zijazo wa miradi nchini Uganda, sababu ikitaja kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu kutokana na hivi karibuni kupitishwa kwa sheria ya kupinga ushoga.