Mapigano yamezuka upya kati ya jeshi la Sudan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) katika jimbo la Darfur Kusini, magharibi mwa Sudan, wakati mapambano ya kikabila yakiendelea jimboni humo.
Kulikuwa na ripoti zenye utatanishi kuhusu idadi ya vifo na majeruhi kutokana na mapigano ya kijeshi na ghasia za kikabila. Taarifa ya kikosi cha RSF imesema, raia zaidi ya 43 wakiwemo watoto na wanawake wanane, wameuawa katika mashambulizi ya kiholela ya mizinga dhidi ya makazi kadhaa huko Nyala, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kusini.
Jeshi la Sudan bado halijajibu shutuma hizo, lakini vyombo vya habari vya huko na mashuhuda, vimesema watu wengi wamepoteza maisha katika mapambano ya kikabila jimboni humo.
Shuhuda mmoja huko Nyara amesema tangu ijumaa iliyopita mapambano yametokea kati ya makabila ya Salamat na Bani Halba, na mwingine amesema mapambano yamepamba moto na kusababisha idadi kubwa ya vifo na majeruhi, huku akiongeza kuwa idadi halisi haiwezi kujulikana kutokana na hali ya usalama.