Somalia na Mashirika ya Umoja wa Mataifa waanza kutoa chanjo ya kipindupindu
2023-08-14 08:36:26| CRI

Serikali ya Somalia na mashirika ya Umoja wa Mataifa wameanzisha kampeni ya siku tano ya kutoa chanjo ya kipindupindu katika wilaya tano za Somalia ikiwahusisha watu laki 5.9 wenye umri wa mwaka mmoja na zaidi wakiwemo akina mama wajawazito.

Wizara ya Afya ya Somalia, Shirika la Afya Duniani (WHO), na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) wamesema kwenye taarifa ya pamoja kuwa tayari kampeni ya kutoa dozi moja ya chanjo ya kipindupindu inaendelea katika Jimbo la Jubaland, kwenye mpaka wa Kenya na Ethiopia, eneo linaloitwa pembetatu ya Mandera.

Waziri wa Afya wa Jimbo la Jubaland Bw. Ismail Ahmed Garas amesema japokuwa mfumo wa afya wa Somalia unaweza kuwa dhaifu, lakini wana azma thabiti ya kuokoa maisha.

Mwakilishi wa WHO nchini Somalia Bw. Mamunur Rahman Malik amesema inawezekana kuwa Somalia itaepuka tishio la njaa, lakini sio tishio la magonjwa kwa sababu ukame wa muda mrefu unaonyesha athari ya kutishia maisha ya watu kote nchini na haswa katika pembetatu ya Mandera.