Juzuu la kwanza la Kitabu cha Utawala wa China Lazinduliwa Nairobi.
2023-08-15 08:53:46| cri

Balozi wa China nchini Kenya Zhou Pingjian, amesifia lugha ya Kiswahili na kuitaja kuwa daraja kati ya China na nchi zinazotumia lugha hii kwa mawasiliano. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa juzuu la kwanza la kitabu cha Utawala wa China kilichoandikwa na rais Xi Jinping, balozi Zhou amesema kuwa kitabu hiki ni picha kamili ya ufanisi wa China. Tom Wanjala na maelezo.

Hafla hii iliyoandaliwa hapo  katika chuo kikuu cha Nairobi, ilihudhuriwa na wageni mashuhuri akiwemo, waziri wa Utalii na Wanyapori  wa Kenya Peninah Malonza, waziri wa Utalii na Utamaduni wa China Hu Heping,  katibu katika wizara ya Elimu, idara ya Elimu ya Msingi Paul Kibet, miongoni mwa wengine.

Mgeni rasmi waziri Malonza alisifu hatua hii ya kutafsiri kitabu cha rais Xi kwa lugha ya Kiswahili, na kuitaja kuwa jukwaa la kuifanya Kenya kupata nguvu na hekima.

“Katika safari yetu isiyo na kikomo katika mambo yanatotuleta pamoja, Kenya na China zimekuwa zikikumbatia tamaduni nyingi kutoka pande zote mbili. Tamaduni hizi zinawapa nguvu watu wetu na kuimarisha undugu na utamaduni.”

Akihutubia kwa niaba ya waziri wa Elimu wa Kenya, katibu katika idara ya Elimu ya msingi Paul Kibet alisema Kenya inaweza kuiga mambo mengi kutoka kwa China, namna ya kuinua kiwango cha elimu na haswa mtaala mpya wa CBC.

“Nchi yetu inaweza ikaiga programu nyingi kutoka kwa China. Kwa mfano, jinsi serikali ya watu wa China imeweza kuboresha kiwango chake cha elimu kwa mamilioni wa raia wake. Kuna mafunzo mengi tunayoweza kujifunza kutoka kwa kitabu cha rais Xi Jinping. Tutazamia kujifunza na kutangamana mara kwa mara.  ”

Balozi wa China nchini Kenya Zhou Pingjian alisisitiza umuhimu na nguvu ya lugha katika mawasiliano. Aliongeza kuwa China inahitaji kujua mengi kuhusu dunia, kama dunia inavyozidi kujua mengi kuhusu China.

Juzuu nne za Xi Jinping zimefungua dirisha kwa jamii za kimataifa kuelewa China zaidi. Usomaji wa  nakala ya kitabu hiki cha Utawala wa China kilichochapishwa kwa lugha ya Kiswahili nchini Kenya na kwingine kitawafanya watu kuelewa zaidi na kuona vyema jinsi China inavyojiendesha. Kwa niaba ya ubalozi wa China nchini Kenya, hapa Nairobi, napongeza idara ya uchapisha vitabu ya KLB na washirika wengine kwa uzinduzi wa juzuu la kitabu hiki.

Mkurugenzi mkuu wa taasisi ya sera za Afrika  profesa Peter Kagwanja ambaye alikuwa mmoja wa wageni waalikwa, alisema kitabu hiki kitawafaa sio tu wananchi, bali pia viongozi wa nchi zinazozungumza Kiswahili.