Bodi ya Chai Kenya (TBK) imesema uuzaji wa chai ya Kenya nje ya nchi umeathiriwa na migogoro inayoendelea nchini Sudan na kati ya Russia na Ukraine, ambapo mauzo yake ya nje ya nusu mwaka yalipungua wakati bei yake duniani inakuwa chini.
Bodi hiyo imesema kipindi kinachoishia Juni ya mwaka huu, Kenya imeuza nje tani laki 1.91 za chai ikiwa na thamani ya takriban dola za kimarekani milioni 432, ikilinganishwa na tani laki 2.43 zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 614 mwaka jana kipindi kama hicho. Imeongeza kuwa pungufu ya asilimia 29 ya thamani ya chai inatokana na mahitaji ya chai ya Kenya kupungua duniani yakiathiriwa na migogoro.