Zanzibar kunufaika na biashara ya Kaboni
2023-08-15 08:48:13| cri

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira nchini Zanzibar Khamis Hamza Khamis amesema Zanzibar inatarajia kunufaika na Biashara ya Kaboni wakati wowote kuanza sasa.

Amesema hayo wakati akijibu maswali ya Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Maryam Azan Mwinyi.

Mhe. Khamis amesema ili kutekeleza suala hilo, watalamu wapo katika hatua za mwisho za kufanya utafiti kwenye maeneo yenye misitu ya asili upande wa Tanzania Zanzibar.

Ameutaja Msitu wa Jozani uliopo Unguja na Ngezi katika Kisiwa cha Pemba kuwa inaweza kutumika kuvuna hewa ya ukaa na kuwapatia faida wananchi wa visiwani humo.

Naibu Waziri huyo ameweka wazi kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar inatarajia kutoa elimu kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na raiya huko Zanzibar ili kuwapa uelewa wa suala hilo nzima.

Amesema kuwa Serikali imeunda kikosi kazi kilichoshirikisha Ofisi ya Rais (TAMISEMI) ambacho kinazunguka nchi nzima kutoa elimu kuhusu hewa ya ukaa hususan katika mikoa ya Tabora, Simiyu, Katavi na Manyara, Katavi na maeneo mengine.

Hivyo, amesema kuwa Serikali imeweka mipango thabiti ya kusimamia na kutathmini biashara hiyo ambapo imetoa mamlaka kwa Kituo cha Kitaifa cha Kufuatilia Kaboni (NCMC) kilichopo mjini Morogoro ambacho kinaratibu na kutoa utaalamu kuhusu gesijoto nchini.

Sambamba na hilo pia imeandaa Kanuni na Mwongozo wa mwaka 2023 kwa ajili ya kusimamia biashara na kuhakikisha inakuwa rasmi kwa wadau ili iwanufaishe na kusaidia katikia utunzaji wa mazingira.