Bei ya mayai yapanda Dar Es Salaam
2023-08-16 09:14:28| cri

Wenyeji wa Dar es Salaam wanaendelea kushuhudia uhaba mkubwa wa mayai kufuatia utagaji mdogo wa kuku unaosababishwa na hali ya hewa ya baridi. Hatua hiyo imesababisha mayai kuwa miongoni mwa bidhaa zilizoongezeka bei na huenda hali hii ikaendelea hadi Desemba mwaka huu kutokana na kuendelea kuongezeka kwa gharama za uendeshaji kwa wafugaji.

Maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam ikiwemo Tegeta, Mbweni, Kinondoni, Tabata, Mabibo na Ubungo umebaini bei ya rejareja ya yai lisilo la kienyeji ni kati ya shilingi 400 hadi 500 kwa baadhi ya maeneo kutoka shilingi 350 kipindi kama hiki mwaka jana. Pia bei ya jumla kwa trei moja imeongezeka kwa kati ya asilimia 40 hadi asilimia 50 ikiuzwa kati ya shilingi 9,500 hadi 11,000 katika kipindi hicho.

Huku bei ya bidhaa hiyo ikiongezeka, baadhi ya wafugaji wanasema ni fursa kwa kujiingizia kipato ili kufanya shughuli zao kwa ufanisi, kwa kuwa ni nadra mayai kufika bei iliyopo sasa.