Bibi mwenye umri wa miaka 99 ahimiza mambo ya utamaduni kijijini
2023-08-16 11:07:32| CRI

Katika maktaba ya Kijiji cha Yuqiao, Mtaa wa Kunlun, mjini Liyang, bibi Chu Juchu, akishikilia orodha ya program na majina ya watu ya mawasiliano, anaelezea kwa furaha shughuli mbalimbali za kitamaduni alizoandaa kwa wazee wa vijijini mwaka huu. Ni vigumu kutambua kuwa ana umri wa miaka 99 kutokana na muonekano wake.

Chu Juchu alizaliwa mwaka 1925, katika familia ya kawaida ya wakulima huko Yixing, mkoani Jiangsu. Alipokuwa na umri wa miaka 21, alihitimu kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Huiwen ya Nanjing na kuwa mwalimu wa shule ya msingi vijijini. Baada ya kustaafu, Chu Juchu akawa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Wazee cha Liyang, ambako alijifunza ngoma ya jadi, muziki, sanaa ya kukata karatasi pamoja na kozi nyingine. Kila siku alisafiri kwa saa mbili kati ya kijiji cha Yuqiao na mji wa Liyang. Alianzisha kikundi cha ngoma cha wazee, na kila alipojifunza aina mpya ya ngoma aliwafundisha wazee wengine.  

Kutokana na kuboreshwa kwa kiwango cha maisha vijijini, idadi ya wazee vijijini inazidi kuongezeka, na kwa kawaida wazee hao hawana sehemu na njia nyingi za kujiburudisha, isipokuwa kutazama vipindi vya televisheni ama kucheza poker. Kutokana na hayo, alipokuwa na umri wa miaka 80, Chu Juchu alipata wazo la kuanzisha maktaba kwa wazee kijijini, ili kuwawezesha wazee kusoma. Baada ya kufanya majadiliano, wakuu wa Kamati ya kijiji cha Yuqiao walikubaliana kukarabati nyumba tatu zisizo na wakazi kuwa maktaba ambayo inasimamiwa na Chu Juchu.

Maktaba hiyo ina vyumba viwili lakini eneo la jumla halizidi mita za mraba 15, lakini bibi Chu amejitolea kwa juhudi kubwa kwa miaka 20 katika kazi ya kubuni na kupanga shughuli mbalimbali, na kuifanya maktaba hiyo si kama tu inawawezesha wazee kusoma, bali imekuwa kituo cha burudani kwa wazee, ambapo wanaweza kuwasiliana na kufanya shughuli mbalimbali za burudani.

Bibi Chu anasema kuwa, baadhi ya watu walimwambia kuwa, umri wake umekuwa mkubwa hivyo si lazima afanye hivyo, anachohitaji ni kujifurahisha tu. Lakini yeye anaona kuwa maana ya maisha ni “kufanya bidii”. Anasema alikuwa mwalimu wa shule ya msingi akiwafundisha watoto ujuzi na elimu, na anapozeeka anataka kujenga jukwaa la kuwafurahisha wazee. Anaona hii ni kazi yenye thamani sana, na kama bado ana nguvu, ataendelea na kazi hiyo.