Mlalamikaji ataka Bunge lipige marufuku matumizi ya TikTok nchini Kenya
2023-08-16 11:08:04| cri

Mlalamikaji amewataka wabunge nchini Kenya kupiga marufuku matumizi ya mtandao wa kijamii wa TikTok akisema kuwa unachangia mmomonyoko wa maadili ya kitamaduni na kidini katika jamii.

Afisa Mtendaji wa Kampuni ya Bridget Connect Consultancy Bob Ndolo katika ombi lake kwa Bunge la Kitaifa, alitoa wito kwa wabunge kuharakisha na kupiga marufuku matumizi ya TikTok nchini humo kwa kuwa inawafanya vijana waone maudhui machafu ya ngono.

Mlalamikaji amekemea kuwa wakati mtandao huo umepata umaarufu miongoni mwa vijana nchini humo, maudhui yanayosambazwa kwenye jukwaa hayafai hivyo basi kuendeleza vurugu, maudhui ya ngono ya wazi, kauli za chuki, lugha chafu na tabia za kuudhi ambazo ni tishio kubwa kwa maadili ya kitamaduni na kidini.

Anasema mtandao nchini Kenya haudhibitiwi na Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya hivyo basi ni vigumu kudhibiti maudhui yanayopakiwa kwenye TikTok.