Sudan Kusini yadhamiria kutimiza ratiba ya uchaguzi licha ya mchakato kuwa polepole
2023-08-16 09:17:08| CRI

Sudan Kusini imeahidi kuwa itatimiza ratiba ya mwezi wa Desemba ya uchaguzi wa mwaka 2024, licha ya kasi ndogo kwenye mchakato wa utekelezaji wa mifumo mikuu ya amani inayohitajika kutimiza upigaji kura wa uhuru, haki na uaminifu.

Waziri wa habari, mawasiliano, teknolojia na huduma ya posta wa nchi hiyo Bw. Michael Makuei, amesema wataendelea na mchakato wa uchaguzi hata kama hawatatekeleza kwa wakati vifungu muhimu vya makubaliano ya amani ya 2018 yaliyorejeshwa.

Bw. Makuei amesema wanaweza kusema wako tayari kwa uchaguzi, na kupuuza baadhi ya watu wanaoona kuwa uchaguzi hautawezekana bila kutekelezwa kwa vifungu vyote vya makubaliano ya amani.

Bw. Makuei amesema hayo kufuatia maoni ya naibu mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu anayeshughulikia suala la Sudan Kusini, akisema kuchelewa kwa utekelezaji wa vigezo vya uchaguzi na katiba kuhusu kurejesha makubaliano ya amani ya mwaka 2018 kumetia shaka uwezekano wa kufanyika kwa uchaguzi huo mwaka 2024.