Kenya yarejesha Ruzuku kwa bei za bidhaa za petrol
2023-08-16 23:13:53| cri

Serikali ya Kenya imelazimika kurejesha mpango wa kutoa ruzuku kwa bei za bidhaa za mafuta ili kuzuia kupanda kwa bei. Serikali ilizamika kudumisha bei za bidhaa za petroli ambazo zimetumika tangu Julai 14, 2023. Mamlaka ya Kudhibiti Bei za Kawi na Bidhaa za Petroli (EPRA) imesema kuanzia Jumanne Agosti 15, 2023, bei za mafuta aina ya petroli, dizeli na mafuta taa hazitabadilia. Bei hizo zitasalia shilingi 194.68 kwa lita moja ya petroli, shilingi 179.67 kwa lita ya dizeli na shilingi 169.48 kwa lita ya mafuta taa jijini Nairobi. Awali, serikali ya Rais William Ruto ilikuwa imetupilia mbali mpango wa kutoa ruzuku kwa bei za mafuta kuanzia Mei 2023, hatua iliyochangia bei za bidhaa za petroli kupanda kwa hadi shilingi 13 kwa lita moja. Kulingana na EPRA, kurejeshwa kwa ruzuku kwa bei za mafuta kunalenga kuwakinga Wakenya kutokana na makali ya kupanda kwa bei kulikochangiwa na kupanda kwa bei za bidhaa hiyo katika masoko ya kimataifa. Hii ina maana kuwa chini ya mpango huu mpya, serikali itaziruzuku Kampuni za Kuuza Mafuta (OMCs) kwa kuweka mkakati wa kutoongeza bei za bidhaa za mafuta.