Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ahimiza kusitishwa kwa mapigano Ethiopia
2023-08-17 07:59:02| CRI

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) Bw. Moussa Faki Mahamat ametoa wito kwa pande zinazopambana nchini Ethiopia kusitisha mapigano na kuhakikisha usalama wa raia.

Wito huo umetolewa kufuatia mapigano ya siku kadhaa yanayoendelea katika miji ya eneo la Amhara, kati ya vikosi vya serikali na wapiganaji wanaojulikana kama Fano.

Kwenye taarifa iliyotolewa jana Bw. Mahamat amesisitiza msimamo wa dhati wa Umoja wa Afrika kuhusu kufuatwa kwa utaratibu wa kikatiba, ukamilifu wa ardhi, umoja na uhuru wa Ethiopia ili kuhakikisha utulivu katika nchi hiyo.

Aidha amezitaka pande zinazozozana katika eneo la Amhara nchini humo kufanya mazungumzo ili kufikia suluhu la amani.

Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) imetoa taarifa ikisema hospitali za huko zinakabiliwa na shinikizo kubwa kutokana na kufurika kwa wagonjwa walio na majeraha yanayohusiana na mapigano katika eneo la Amhara.