Wang Yi ahutubia ufunguzi wa Maonesho ya 7 ya China na Asia Kusini
2023-08-17 10:57:24| cri

Mkurugenzi wa ofisi ya mambo ya nje ya kamati kuu ya chama cha Kikomunisti cha China, Wang Yi alihudhuria na kuhutubia sherehe ya ufunguzi wa maonesho ya saba kati ya China na nchi za Asia ya kusini yanayofanyika mjini Kunming, mkoani Yunnan kusini magharibi mwa China.

Bw. Wang alisema, mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 10 ya maonesho hayo, pia ni maadhimisho ya miaka 10 ya Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja na wazo la kidiplomasia la nchi jirani linalojumuisha upendo, udhati, kunufaishana na ushirikishwaji. 

Wang alibainisha kuwa katika miaka 10 iliyopita, wameimarisha mshikamano na ushirikiano katika kulinda usalama wa kikanda na mazingira ya maendeleo. Pia wameendelea kujenga Ukanda Mmoja, Njia Moja na kupata mafanikio makubwa katika muunganisho, miundo mbinu, biashara na uwekezaji, na sekta nyingine. Halikadhalika wamefanya mabadilishano ya kina ya kirafiki, kufuata kanuni ya uwazi na kujumuishana, na kujenga jukwaa la ngazi mbalimbali la mabadilishano kati ya watu na watu.

Alisisitiza kwamba, China iko tayari kushirikiana na nchi za Asia ya kusini katika kuimarisha mshikamano na ushirikiano, kukuza nguvu mpya za maendeleo, kujenga jumuiya yeynye maendeleo ya pamoja, na kutoa mchango katika kudumisha amani, utulivu na ustawi wa kanda hiyo.

Waziri Mkuu wa Sri Lankan Bw. Dinesh Gunawardena, Makamu wa Rais wa Laos Pany Yathotou, Makamu wa Rais wa Nepal Ram Sahay Prasad Yadav, na Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam Bw. Tran Luu Quang walihudhuria ufunguzi huo.