Afrika ina kiwango cha juu zaidi cha wajasiriamali duniani, na pia ni bara pekee ambalo lina wanawake wajasiriamali wengi, hiyo ni kwa mujibu wa Benki ya Dunia mwaka 2019. Vilevile, Afrika ina utamaduni wa muda mrefu wa wafanyabiashara wa kike, na mifano ipo mingi. Wanawake hawa sio tu wanajishughulisha na biashara barani humo, bali sasa wamevuka mipaka ya nchi na bara na kufika hadi hapa China wakiendesha biashara zao.
Baadhi yao wanafanya biashara wao wenyewe, ila wengine wamebahatika hadi kuolewa na wenyeji tukimaanisha Wachina. Ingawa watu wengi huwa wanajiuliza kama ndoa kati ya Wachina na Waafrika inawezekana. Lakini ukweli umedhihirisha kwamba ni jambo linalowezekana kabisa. Wengi wa wanawake wa Afrika wanaoishi na kuolewa na Wachina wanasema maisha yao kwa ujumla ni mazuri, hata hivyo changamoto mbili tatu hazikosekani kwani hata ukiolewa na mwafrika mwenzio pia changamoto hizi hujitokeza tena pengine zinaweza kuwa kubwa zaidi.
Hivi karibuni mwenzangu Pili alibahatika kushuhudia kwa macho yake ndoa kati ya Mchina na mwanamke wa Afrika, ambapo leo hii ndio itakuwa mada yetu kuu kwenye Ukumbi wa Wanawake ambapo tutaangalia Wajasiriamali wanawake wa Afrika wanavyoendesha biashara zao nchini China na ndoa zao kwa Wachina.