Waziri wa mambo ya nje wa Misri na Mjumbe wa UM wajadili mgogoro wa Syria
2023-08-21 09:16:07| CRI

Waziri wa mambo ya nje wa Misri Sameh Shoukry na Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa Bw. Geir O. Pedersen wamejadili kuhusu hali mpya nchini Syria.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Misiri, kupitia mazungumzo ya simu, Shoukry na Pedersen wamejadili kuhusu matokeo ya mkutano wa kwanza wa kamati ya mawasiliano ya mawaziri wa nchi za Kiarabu kuhusu Syria uliofanyika huko Cairo Agosti 15.

Kamati hiyo iliyoundwa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu AL, ina mawaziri wa mambo ya nje wa Misri, Saudi Arabia, Jordan, Iraq, Lebanon na mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.

Waziri wa mambo ya nje wa Misri amesisitiza kuwa kamati hiyo inatarajia kufikia utatuzi kuhusu mgogoro wa Syria na kulinda umoja na utulivu wa Syria.

Taarifa hiyo pia imesema, Shoukry na Pedersen wamekubaliana kufanya mkutano wa pande mbili kando ya vikao vya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwezi wa Septemba.