Waziri wa Mambo ya Nje asema China na Iran zitasaidiana katika maslahi ya msingi
2023-08-21 09:15:14| CRI

Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi amesema China iko tayari kuendelea kushirikiana na Iran ili kusaidiana kithabiti katika masuala yanayohusu maslahi ya msingi.

Akiongea kwa njia ya simu na mwenzake wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian jana Jumapili, Bw Wang aliongeza kuwa wakati Rais Ebrahim Raisi wa Iran alipofanya ziara ya kiserikali nchini China mwezi Februari mwaka huu, wakuu wa nchi hizi mbili walifikia makubaliano mapya muhimu kuhusu ushirikiano wa pande mbili, jambo ambalo lilipelekea uhusiano wa China na Iran kufikia ngazi mpya.

Aidha Bw. Wang amesema China pia iko tayari kuendelea kushirikiana na Iran kupinga kwa pamoja uingiliaji kati wa nje, kupinga uonevu wa upande mmoja, kutetea mamlaka, usalama na maslahi ya maendeleo ya nchi hizo mbili na kulinda maslahi ya pamoja ya nchi zinazoendelea na haki ya kimataifa.

Naye Amir-Abdollahian amesema, Iran inatilia maanani sana maendeleo ya ushirikiano wa kina wa kimkakati kati ya Iran na China, na inatazamia kudumisha mawasiliano ya hali ya juu na China, kuzidisha ushirikiano chini ya Pendekezo la ‘Ukanda Mmoja Njia Moja’ na kuimarisha uratibu na ushirikiano katika masuala ya kimataifa na kikanda.