Rais Xi Jinping wa China afanya mazungumzo na rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini
2023-08-22 21:07:48| CRI

Rais Xi Jinping wa China amefanya mazungumzo na mwenzake wa Afrika Kusini rais Cyril Ramaphosa katika mji wa Pretoria leo asubuhi kwa saa za huko.

Rais Xi amesema kuwa hii ni ziara yake ya nne nchini Afrika Kusini akiwa rais wa China. China inafurahi kuona ujenzi wa taifa la Afrika Kusini na ushawishi wake wa kimataifa kuendelea kupanda na kutarajia nchi hiyo kupiga hatua zaidi katika maendeleo yake. Katika miaka kumi iliyopita, ameshuhudia kustawi kwa uhusiano kati ya China na Afrika Kusini ambapo ameshuhudia kuanzishwa kwa taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Durban, kujionea mvuto wa shughuli za “Mwaka wa China” nchini humo na pia alibonyeza kitufe cha kuanzisha uzalishaji wa kiwanda cha BAIC nchini Afrika Kusini pamoja na rais Ramaphosa.

Rais Xi ameeleza kuwa uhusiano mzuri na urafiki mkubwa kati ya China na Afrika Kusini unatokana na pande hizo mbili kushikana mkono wakati wa dhiki na faraja katika njia zao za maendeleo. Sasa katika mwanzo mpya wa kihistoria, kuendeleza na kuimarisha urafiki na ushirikiano huo ni matarajio ya pamoja ya nchi hizo mbili na pia ni jukumu muhimu la pamoja katika zama za leo. Rais Xi amesema yuko tayari kufanya juhudi pamoja na rais Ramaphosa katika kuhimiza uhusiano huo wa kimkakati wa pande zote ufikie ngazi mpya.