Idadi ya abiria wa SGR nchini Kenya yaongezeka kwa asilimia 15 katika robo ya kwanza ya mwaka huu
2023-08-22 09:12:00| CRI

Shirika la Reli la Kenya (KRC) limesema kuwa idadi ya abiria waliotumia huduma ya treni ya reli ya kasi, SGR katika robo ya kwanza ya mwaka huu ilipanda kwa takriban asilimia 15.2 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Ripoti imesema kuwa treni hiyo katika muda wa miezi mitatu ilisafirisha abiria 597,506, wakiongezeka kutoka abiria 518,780 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Ongezeko la idadi ya abiria lilishuhudia treni hiyo, ijulikanayo kama Madaraka Express, ikirekodi ongezeko kubwa la mapato hadi takriban shilingi milioni 661 (kama dola za Kimarekani milioni 4.58) katika robo ya kwanza, ikiwa ni ongezeko kutoka dola milioni 3.9 ikilinganishwa na miezi mitatu ya kwanza ya mwaka jana.

Kuongezeka kwa mahitaji ya huduma ya treni kunaonyesha kuwa wasafiri wengi wa Kenya wanatafuta usafiri wa kuaminika, wanaoumudu, na wa kasi, wakati wanaposafiri kati ya Nairobi, mji mkuu wa Kenya, na Mombasa, kivutio cha watalii cha pwani.