Mvua za El Nino kunyesha Pembe ya Afrika katika robo ya mwisho ya mwaka huu
2023-08-23 22:54:11| cri

Shirika la Maendeleo la Serikali za Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) limesema, kanda ya Pembe ya Afrika huenda ikashuhudia mvua kubwa kuanzia mwezi Oktoba hadi Desemba zinazohusishwa na hali ya hewa ya El Nino.

Katika ripoti yake kuhusu utabiri wa hali ya hewa iliyotolewa jana jumanne mjini Nairobi, Kenya, Shirika hilo limesema kuna uwezekano wa asilimia 80 wa mvua kubwa kunyesha katika kipindi hicho kwenye Pembe ya Afrika, hususan maeneo ya kusini mwa Ethiopia, mashariki mwa Kenya, na kusini mwa Somalia.

Mkurugenzi wa Kituo cha Utabiri wa Hali ya Hewa (ICPAC) kilicho chini ya IGAD, Guleid Artan amesema, mvua hizo zitaleta nafuu kwa wakulima wadogo na wafugaji katika Pembe ya Afrika ambao wamekabiliwa na ukame mkali kwa miaka mitatu mfululizo.

Pia ameonya kuwa, mvua hizo zinaweza kusababisha uvamizi wa wadudu kama nzige wa jangwani, maporomoko ya udongo na mafuriko ya ghafla, na hivyo kufanya hali kuwa mbaya zaidi kwa jamii ambazo tayari zinakabiliwa na athari mbaya ya mabadiliko ya tabianchi.