Waziri wa Afya awataka Watanzania kujenga utamaduni wa kupima afya
2023-08-23 10:57:52| cri

Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amewataka Watanzania kujengea tabia ya kupima afya mara kwa mara badala ya kusubiri hadi waugue, kwani kufanya hivyo kutasaidia kuepuka gharama kubwa za matibabu.

Akizungumza katika ufunguzi wa kambi ya upimaji afya itakayofanyika kwa siku tano jijini Tanga kuanzia jana jumanne, Waziri Ummy amesema, mazoea ya kutopima afya ni mabaya kwani yamewasababishia watu wengi matatizo ya kutopata matibabu yanayostahili kwa wakati na yenye gharama.

Amewataka Watanzania kufanya mazoezi ya miili ikiwa pamoja na kutembea, kukimbia au hata kuzunguka nyumba zao mara kadhaa, na kuwasisitiza kuepuka vyakula vyenye chumvi nyingi.