EAC yaanza mazungumzo kuhusu uanachama wa Somalia
2023-08-23 10:05:13| CRI

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Jumanne ilianza mazungumzo mjini Nairobi nchini Kenya, ili kuiingiza Somalia katika jumuiya hiyo ya kiuchumi ya kikanda.

Peter Mathuki, katibu mkuu wa jumuiya hiyo ya kiserikali, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mazungumzo hayo ni ya hatua ya mwisho kabla ya Somalia kujiunga na EAC. Amebainisha kuwa watawasilisha ripoti ya mazungumzo kwenye baraza la mawaziri pamoja na kikao cha wakuu wa nchi za EAC kabla ya mwisho wa mwaka.

Waziri wa Mipango, Uwekezaji na Maendeleo ya Uchumi wa Somalia, Mohamud Abdirahman Sheikh Farah, alisema kuwa nchi yake ina nia ya kujiunga na EAC kwa sababu tayari ina uhusiano wa karibu wa kijamii na kiuchumi na nchi zote wanachama wa jumuiya hiyo ya kibiashara. Pia amesema wamepata mapokezi mazuri kutoka kwa wakuu wa nchi wanachama wote wa EAC.

Nchi wanachama wa EAC ni pamoja na Burundi, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na Uganda.