Uganda yatoa chanjo ya virusi vya Ebola kwa wahudumu wa afya walio mstari wa mbele katika eneo la kaskazini magharibi
2023-08-23 10:05:45| CRI

Uganda imeanza zoezi la kutoa chanjo ya Ebola jana Jumanne ikianza na wahudumu wa afya walio mstari wa mbele 2,500 katika wilaya ya Adjumani katika eneo lake la kaskazini-magharibi mwa Nile inayopakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Sudan Kusini.

Henry Lulu, afisa wa afya wa wilaya ya Adjumani, aliiambia Xinhua kwa njia ya simu kwamba zoezi hilo linaanza na wafanyakazi wa afya walio mstari wa mbele na baadaye litaendelea kwa umma. Amefafanua kuwa wakati wakizindua zoezi hili jana, wamepokea dozi 400 za chanjo kwa wilaya ya Adjumani, na kwamba dozi nyingi zaidi za chanjo zitapelekwa katika wilaya zote sita za ukanda wa Nile Magharibi.

Diwani wa Wilaya ya Adjumani Irene Adrupio pia aliiambia Xinhua kuwa wahudumu wa afya walio mstari wa mbele wanaokoa maisha ya watu kwanza, hivyo ni muhimu kuwaweka salama na kufanya kazi zao za kawaida bila hofu ya kuambukizwa na magonjwa.

Disemba mwaka jana, Uganda ilipokea dozi 1,200 za chanjo ya majaribio ya Ebola kutoka Shirika la Afya Duniani kwa ajili ya majaribio ya kimatibabu yenye lengo la kupambana na virusi vya Ebola vilivyoikumba nchi hiyo mwezi Septemba.