Rais wa China afanya mazungumzo na mwenzake wa Afrika Kusini
2023-08-23 09:40:58| CRI

Rais Xi Jinping wa China ambaye yuko ziarani Afrika Kusini amefanya mazungumzo na mwenzake wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa katika Ikulu huko Pretoria. Marais hao wawili wamebadilishana maoni juu ya maendeleo ya uhusiano kati ya China na Afrika Kusini na masuala ya kimataifa na kikanda yanayofuatiliwa na pande mbili, huku wakifikia makubaliano muhimu ya kuhimiza uhusiano wa kimkakati na kiwenzi wa pande zote kati ya nchi mbili katika kiwango cha juu zaidi na kujenga jumuiya yenye mustakabali wa pamoja ya hali ya juu kati ya pande mbili.

Rais Xi amesema, China inapenda kushirikiana na Afrika Kusini katika kurithisha urafiki, kuimarisha ushirikiano, na kuzidisha uratibu. Ili kuhimiza uhusiano wa kimkakati na kiwenzi wa pande zote katika ngazi mpya na kujenga jumuiya yenye mustakabali wa pamoja ya hali ya juu kati ya pande mbili, rais Xi ametoa mapendekezo manne.

La kwanza, China na Afrika Kusini zinatakiwa kuwa wenzi wa kimkakati wenye hali ya juu ya kuaminiana. La pili, China na Afrika Kusini zinatakiwa kuwa wenzi wa maendeleo wanaopiga hatua kwa pamoja. La tatu, China na Afrika Kusini zinatakiwa kuwa wenzi wa kirafiki wanaoelewana na kupendana. La nne, China na Afrika Kusini zinatakiwa kuwa wenzi wa dunia nzima wanaolinda haki.

Rais Xi pia amesisitiza kuwa China na Afrika siku zote ni jumuiya yenye hatima ya pamoja. Wakati zikikabiliana na changamoto mbalimbali za dunia, pande mbili za China na Afrika zinatakiwa kuimarisha zaidi umoja na ushirikiano kuliko wakati wowote. China inaunga mkono kithabiti nchi za Afrika kuungana na kujitegemea na kuunga mkono kithabiti Umoja wa Afrika kujiunga na kundi la nchi 20 na pia kuunga mkono kithabiti Afrika kuhimiza mchakato wa utandawazi wa viwanda na kilimo wa kisasa.

Rais Ramaphosa amesema, anafurahia kumpokea rais Xi kwa ziara yake ya nne nchini Afrika Kusini. China imetoa uungaji mkono muhimu katika mchakato wa Afrika Kusini kujipigania uhuru na kutimiza maendeleo ya taifa, na kutoa msaada katika wakati mgumu wa maambukizi ya COVID-19. China ni ndugu, rafiki na mwenzi wa dhati. Nchi hizo mbili zote zinatafuta ustawi na maendeleo ya taifa na kuwa na misimamo inayofanana katika mambo mengi muhimu ya kimataifa. Afrika Kusini pia imekipongeza chama cha kikomunisiti cha China CPC kwa kuwaongoza watu wa China kupata maendeleo makubwa, ikipenda kuimarisha mawasiliano kati ya vyama vya kisiasa, kuzidi kubadilishana uzoefu wa utawala, kuanzisha ushirikiano wa majaribio wa kupunguza umaskini kwa njia inayotumiwa na China, kuongeza ushirikiano katika sekta za biashara, uwekezaji, nishati, ujenzi wa miundombinu, utengenezaji na sayansi na teknolojia na kukaribisha makampuni mengi zaidi ya China kuwekeza na kuanzisha shughuli zao nchini humo.