Rais wa China ahimiza BRICS kuboresha usimamizi wa mambo ya kimataifa
2023-08-24 15:47:44| cri

Mkutano wa 15 wa viongozi wa BRICS jana umefanyika mjini Johannesburg, Afrika Kusini. Rais wa China Xi Jinping, amesema nchi za BRICS ni nguvu muhimu katika kuunda usimamizi wa mambo ya kimataifa, na zinapaswa kutoa uhakika, utulivu na nguvu chanya zaidi kwa dunia.

Katika mkutano huo, viongozi wa nchi tano za BRICS wamekubaliana kwamba dunia ya sasa imeingia katika kipindi kipya cha mabadiliko. Rais Xi amesema, nchi za BRICS zimechagua kwa uhuru njia ya kujiendeleza, kutetea kwa pamoja haki ya maendeleo, na kuelekea kutimiza mambo ya kisasa, na huu ni mwelekeo wa jamii ya binadamu, na utaathiri sana mchakato wa maendeleo ya dunia.

Rais Xi ameeleza kuwa ushirikiano wa BRICS uko katika kipindi muhimu, nchi wanachama wake zinapaswa kushikamana na kushikilia nia yao ya awali ya kujiletea maendeleo kupitia umoja, kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali, na kuhimiza mageuzi ya mifumo ya usimamizi wa mambo ya kimataifa, ili iwe haki na kuwa na usawa zaidi.

Kuhusu ushirikiano wa uchumi, rais Xi amependekeza kuwa nchi za BRICS zinapaswa kuwa washirika katika maendeleo na ufufuaji wa uchumi, na kupinga vitendo vya “kutenganishana kiuchumi na kuvunja mnyororo wa ugavi”. Pia amependekeza kuimarisha ushirikiano katika uchumi wa kidijitali, maendeleo ya kijani, mnyororo wa ugavi na sekta nyingine.

Kuhusu usimamizi wa mambo ya kimataifa, rais Xi amesema nchi za BRICS zinapaswa kufuata mfumo wa kweli wa pande nyingi, kuhimiza mageuzi ya usimamizi wa mambo ya kimataifa, na kuongeza uwakilishi na sauti ya nchi zinazoendelea.