Xi asema BRICS ni nguvu muhimu katika kuunda mazingira ya kimataifa
2023-08-24 09:43:09| CRI

Rais Xi Jinping wa China Jumatano alitoa hotuba kwenye mkutano wa kilele wa 15 wa BRICS unaofanyika huko Afrika Kusini akisema kwamba BRICS ni nguvu muhimu katika kuunda mazingira ya kimataifa.

Kwenye hotuba hiyo amesisitiza kuwa nchi za BRICS zinachagua njia zao za maendeleo kwa uhuru, kulinda kwa pamoja haki yao ya maendeleo, na kusonga mbele kuelekea kwenye hali ya usasa, ambayo inawakilisha mwelekeo wa maendeleo ya jamii ya binadamu, na itaathiri sana mchakato wa maendeleo duniani. Historia ya BRICS inaonesha kuwa wanachama wamechukua hatua mara kwa mara kwa moyo wa BRICS wa uwazi, ushirikishwaji na kuwa na ushirikiano wa kunufaishana, na kuupeleka ushirikiano wa BRICS katika viwango vipya vya kuunga mkono maendeleo ya nchi tano.

Akizungumzia suala la uchumi, rais Xi alitoa wito wa kufanywa juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kifedha kati ya nchi za BRICS ili kukuza ukuaji wa uchumi. Amesema kufufuka kwa uchumi wa dunia bado kupo kwenye hali ya kutetereka, na changamoto kwa nchi zinazoendelea ni kubwa zaidi, zikikwamisha juhudi zao za kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu. Ametilia mkazo kwamba “Maendeleo ni haki isiyoweza kubatilishwa ya nchi zote, na si fursa iliyohifadhiwa kwa wachache”.

Rais Xi pia alitoa mapendekezo ya China kwa nchi za BRICS, kwamba zipanue ushirikiano katika elimu, kuongeza jukumu la muungano wa BRICS kwenye elimu ya ufundi stadi, kuchunguza na kuweka utaratibu wa ushirikiano kuhusu elimu ya kidijitali, na kuhimiza dhana ya ushirikiano wa pande zote kuhusu elimu.