Wanafunzi 80 wa Rwanda wapata udhamini wa masomo wa China
2023-08-24 09:39:53| CRI

Ofisa wa ubalozi wa China nchini Rwanda Jumatano alisema serikali ya China imewapatia wanafunzi 80 wa Rwanda udhamini wa masomo mwaka huu, ili waweze kupata elimu ya juu nchini China, idadi ambayo imekuwa kubwa zaidi katika miaka ya karibuni.

Wanafunzi 75 kati yao watasomea shahada ya uzamili, wawili shahada ya uzamivu na wengine watatu watasomea shahada ya kwanza, ambao watasoma kozi za sayansi, teknolojia, uchumi na nyinginezo.

Balozi wa China nchini Rwanda Bw. Wang Xuekun akihutubia hafla ya kuwaaga wanafunzi hao mjini Kigali aliwahimiza kutumia vizuri fursa hii na kupata maendeleo makubwa kimasomo. Pia aliwahamasisha wanafunzi hao waunganishe lengo lao binafsi na maendeleo ya nchi.

Mkurugenzi mkuu wa Baraza la elimu ya juu la Rwanda Bi. Rose Mukankomeje alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya China na Rwanda kwenye masuala ya ujenzi wa uwezo. Aliwashauri wanafunzi hao kukumbatia utamaduni na jamii ya China, na kutoa mchango kwa maendeleo ya nchi wakati watakaporudi nyumbani baada ya kuhitimu masomo yao.