Mwanadiplomasia mwandamizi wa Afrika Kusini: Nchi za BRCIS kuimarisha ushirikiano na Afrika kutanufaisha pande zote mbili
2023-08-25 08:17:40| CRI

Mkutano wa 15 wa viongozi wa nchi za BRICS uliofanyika kuanzia tarehe 22 hadi 24 mwezi Agosti huko Johannesburg nchini Afrika Kusini ulifuatiliwa sana na jumuiya ya kimataifa. Mwanadiplomasia mkongwe wa Afrika Kusini Gert Grobler alipohojiwa hivi karibuni na Shirika Kuu la Utangazaji la China (CMG), amesema mkutano huo utazisukuma mbele nchi za BRICS kupiga jeki ushirikiano na nchi za Afrika, na kutoa msukumo mpya kwenye maendeleo ya uhusiano kati ya Afrika na China.  


Balozi Gert, ambaye pia ni mtafiti mwandamizi wa Taasisi ya Utafiti wa Afrika katika Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang, amesema ukuaji wa mfumo wa BRICS si kama tu unanufaisha nchi za BRICS pekee, bali pia unanufaisha jumuiya ya kimataifa. Nchi za BRICS siku zote zimekuwa zikijitahidi kuhimiza maendeleo ya pamoja ya nchi zote za Kusini duniani, zikiwemo zile za Afrika, ili nchi yoyote isiachwe nyuma kimaendeleo. Anaona kuwa kaulimbinu ya mkutano wa kilele wa BRICS ambayo ni “BRICS na Afrika: Kukuza Ushirikiano, Kuhimiza Ukuaji wa Pamoja, Kutimiza Maendeleo Endelevu, na Kuimarisha Mfumo Shirikishi wa Pande Nyingi”, inadhihirisha kuwa Afrika Kusini inatarajia kukuza ushirikiano kati ya BRICS na Afrika, na kusukuma mbele zaidi Agenda ya Maendeleo ya Afrika. Balozi Gert amesema, nchi za BRICS kupanua ushirikiano na Afrika kutanufaisha pande zote mbili, na anatarajia kuwa nchi hizo zitanufaika na fursa zinazotokana na ujenzi wa Eneo la Biashara Huria la Bara Afrika, AfCFTA.


Balozi Gert anaona kuwa, China ikiwa ni nchi kubwa zaidi kiuchumi miongoni mwa nchi za BRICS, iko mbioni kujijenga kuwa nchi ya kisasa kupitia maendeleo yenye ubora wa hali ya juu, hali ambayo itaendelea kutoa fursa kubwa za biashara na uwekezaji kwa nchi za Afrika ikiwemo Afrika Kusini na nchi nyingine nyingi duniani. China ni mwenzi mkubwa wa kwanza wa biashara kwa Afrika, mwaka 2022 thamani ya biashara kati ya pande hizo mbili ilifikia dola za kimarekani bilioni 282, na inaendelea kukua. Balozi Gert amesema, hatua mbalimbali zilizochukuliwa na China za kuhimiza uuzaji wa bidhaa za Afrika kwenye soko la China, ikiwemo kuzisaidia nchi za Afrika kuongeza thamani ya bidhaa zao, zina umuhimu mkubwa kwa Afrika. Afrika inaikaribisha China kwa mikono miwili kushiriki kwenye ujenzi wa Eneo la Biashara Huria la Bara Afrika, na pia inatarajia kuwa pande hizo mbili zitaendelea kupanua ushirikiano kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo biashara, uwekezaji na miundombinu.