China yaazimia kukuza mafungamano ya kiuchumi ya Afrika
2023-08-25 09:12:15| CRI

China imeazimia kukuza mafungamano ya kiuchumi ya Afrika kwa kuimarisha na kuunganisha biashara ya ndani ya Afrika, kukuza uwekezaji na kuwezesha maendeleo ya minyororo ya thamani.

Hayo yamo kwenye taarifa ya pamoja iliyotolewa jana Alhamisi huko Johannesburg, Afrika Kusini, baada ya Mazungumzo ya Viongozi wa China na Afrika. Taarifa imebainisha kuwa upande wa Afrika unaipongeza China kwa kuanzisha Mpango wa Maendeleo ya Dunia, Mpango wa Usalama wa Dunia, na Mpango wa Ustaarabu wa Dunia, ili kuunga mkono uimarishaji wa ushirikiano wa pande nyingi na kuamini kuwa maendeleo ya China na Afrika yataleta fursa nyingi zaidi za amani na maendeleo duniani.

Pande zote mbili zitaendelea kuunganisha ushirikiano wa hali ya juu wa Ukanda Mmoja, Njia Moja kati ya China na Afrika, pamoja na Ajenda ya 2063 ya Umoja wa Afrika na mikakati ya maendeleo ya kitaifa ya nchi za Afrika, ili kuinua ushirikiano kati ya China na Afrika katika ngazi za juu. Taarifa hiyo iliongeza kuwa pande zote mbili zilisisitiza dhamira yao ya kuendeleza zaidi ujenzi wa taasisi ya Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).