Rais Xi Jinping wa China akutana na wenzake wa Jamhuri ya Congo, Malawi na Namibia
2023-08-25 09:10:43| CRI

Rais Xi Jinping wa China tarehe 24 Agosti alikutana na wenzake wa Jamhuri ya Congo Denis Sassou Nguesso, Lazarus Chakwera wa Malawi na Hage Geingob wa Namibia kando ya mkutano wa 15 wa wakuu wa nchi za BRICS huko Johannesburg nchini Afrika Kusini.

Alipokutana na Sassou, Xi alisema China inaishukuru Jamhuri ya Congo kwa kuiunga mkono kithabiti China juu ya masuala yanayohusiana na maslahi makuu ya China, na itaendelea kuiunga mkono kithabiti Jamhuri ya Congo katika kulinda uhuru na kujiamulia kwa nchi, kupinga nguvu za nje kuingilia mambo ya ndani, na kuiunga mkono Jamhuri ya Congo kufanya kazi kubwa zaidi kwenye mambo ya kimataifa na ya kikanda. Mwakani itatimia miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya nchi mbili, hivyo China inapenda kushirikiana na Jamhuri ya Congo katika kuhimiza uhusiano wa kiwenzi na ushirikiano wa kimkakati wa pande zote kati ya nchi mbili upate matokeo mengi zaidi.

Kwa upande wa Jamhuri ya Congo, Sassou alisema nchi yake inapenda kuhimiza mawasiliano na ushirikiano na China kwenye mambo ya kimataifa, na kulinda kwa pamoja maslahi ya nchi zinazoendelea.

Kwenye mazungumzo kati ya Xi na Chakwera, Xi alisema China inaiunga mkono Malawi katika kutafuta njia ya maendeleo inayoendana na hali halisi ya nchi, China inataka kuendelea kuipatia Malawi msaada wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. China inapenda kuimarisha mshikamano na ushirikiano na nchi zinazoendelea ikiwa ni pamoja na Malawi, na kuhimiza utaratibu wa kimataifa uendelee ukielekea upande wa usawa na haki zaidi.

Chakwera alisema Malawi inashikilia kithabiti sera ya kuwepo kwa China Moja. Pendekezo la ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” lililotolewa na rais Xi linaweza kusaidia nchi zinazoendelea zitimize maendeleo ya pamoja. Malawi inapenda kuzidi kuhimiza urafiki na ushirikiano na China.

Wakati huohuo, Xi alikutana na mwenzake wa Namibia Hage Geingob. Xi alisema China inapenda kuimarisha ushirikiano na Namibia kwenye sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na nishati safi, kuhamasisha makampuni ya China yawekeze nchini Namibia, kudumisha mawasiliano ya karibu na Namibia, na kuimarisha kwa pande zote uhusiano kati ya nchi mbili.

Geingob alisema Namibia inaiunga mkono kithabiti China, na kukaribisha makampuni mengi ya China yawekeze nchini Namibia. Aidha nchi yake inapenda kushirikiana na China katika kuhimiza uhusiano kati ya nchi hizo mbili upate maendeleo makubwa zaidi.