Xi azihimiza China na Afrika kushirikiana kuhimiza mambo ya kisasa
2023-08-25 09:11:45| CRI

Rais Xi Jinping wa China Alhamisi alitoa hotuba muhimu kwenye Mazungumzo ya Viongozi wa China na Afrika yaliyofanyika huko Johannesburg, Afrika Kusini na kuzitaka China na Afrika kushikana mikono kwa ajili ya kuhimiza mambo ya kisasa.

Amesema China inapenda kuzindua Mpango wa Kusaidia Maendeleo ya Viwanda barani Afrika, ambao utasaidia Afrika katika kukuza sekta yake ya viwanda na kufikia ukuaji wa viwanda na uchumi mseto.

Mpango huo umesisitiza kuwa kupitia programu tisa zilizo chini ya Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika, Ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja na Mpango wa Maendeleo wa Dunia, China itaelekeza rasilimali zaidi za misaada, uwekezaji na ufadhili kwenye programu za uanzishaji wa viwanda.

Aidha amefafanua kuwa China itazindua Mpango wa China wa Kusaidia Uboreshaji wa Kilimo cha kisasa wa Afrika, na kwamba itaisaidia Afrika kupanua mashamba ya nafaka na kuhimiza makampuni ya China kuongeza uwekezaji wa kilimo barani Afrika.

Mpango huo unalenga kusaidia Afrika kufikia kujitosheleza kwa chakula na maendeleo endelevu ya kujitegemea, kukuza uzalishaji wa chakula barani Afrika, kuimarisha uwezo wa Afrika wa kulinda usalama wake wa chakula, na kuisaidia kufikia malengo yanayohusiana katika kuboresha kilimo.

Ameongeza kuwa, China pia itatekeleza mpango wa ushirikiano wa kuwaandaa watu wenye ujuzi kati ya China na Afrika. China inapanga kuisaidia Afrika kutoa mafunzo kwa wakuu na walimu 500 wa vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi vya Afrika na watu wenye ustadi na ujuzi wa lugha ya kichina zaidi elfu 10 kila mwaka.