Rais wa Tanzania asema ushirikiano wa BRICS na Afrika ujikite kufungua fursa muhimu katika bara hilo
2023-08-25 10:29:07| cri

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amesema kutokana na kuongezeka kwa changamoto duniani, kuna haja ya kuwa na majadiliano mapana yenye lengo la kutafuta suluhisho kwa changamoto hizo.

Rais Samia amesema hayo jana Alhamis mjini Johannesburg, Afrika Kusini, wakati akihutubia mkutano wa BRICS uliowakutanisha viongozi kutoka mataifa zaidi ya 50 duniani, zikiwemo nchi wanachama wa kundi hilo ambazo ni Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini. Amesema jambo muhimu ni kuwa na mazungumzo na kuchukua hatua kukabiliana na changamoto hizo ili kukuza uwezo wa kifedha, uwekezaji, biashara na ushirikiano wa kiuchumi.

Rais Samia amesema BRICS inatoa nafasi ya kuja na mikakati ya haki na usawa katika kushughulia masuala ya kiuchumi kupitia ushirikiano wake na bara la Afrika, na kwamba matarajio ya Tanzania ni kuona masuala ya Afrika na vipaumbele vyake yanaendelea kuchukua nafasi kwenye mikutano ijayo ya BRICS.