Nchi sita zatarajia kuimarisha ushirikiano baada ya kualikwa kujiunga na BRICS
2023-08-25 09:13:18| CRI

Mkutano maalumu na wanahabari wa mkutano wa 15 wa wakuu wa nchi za BRICS umetangaza kuzialika Saudi Arabia, Misri, UAE, Argentina, Iran na Ethiopia kujiunga rasmi na mfumo wa nchi za BRICS. Viongozi na maofisa wa nchi hizo sita wamepongeza mwaliko huo na kutarajia kuimarisha ushirikiano zaidi.

Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Faisal bin Farhan amesema, nchi hiyo inatarajia kufanya ushirikiano mwingi zaidi na nchi za BRICS. Amesema, Saudi Arabia ina uhusiano wa kimkakati na nchi za BRICS, mfumo wa BRICS ni njia muhimu ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi mbalimbali, na Saudi Arabia inapongeza nchi za BRICS kuialika nchi hiyo kujiunga na mfumo huu.

Naye Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri ameipongeza Misri kwa kualikwa kujiunga na mfumo huo. Amesema, nchi hiyo inatarajia kufanya uratibu na ushirikiano na nchi wanachama wa sasa na wapya wa nchi za BRICS, ili kutimiza lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi wanachama, kuinua sauti ya nchi za kusini juu ya masuala na changamoto mbalimbali zinazozikabili, na kuhimiza maslahi ya nchi zinazoendelea.

Kwa upande wake Rais Sheikh Mohammed bin Zayed wa UAE amesema kwenye mitandao ya kijamii kuwa, nchi hiyo inakubali mitazamo ya pamoja ya viongozi wa nchi za BRICS kuhusu maendeleo ya siku za baadaye ya binadamu, huku akipongeza uamuzi wa kuialika UAE kujiunga na mfumo wa nchi za BRICS. Nchi hiyo inatarajia kuendelea kuimarisha ushirikiano ili kutimiza ustawi wa pamoja wa dunia nzima.

Rais Alberto Fernandez wa Argentina ametoa hotuba kwa njia ya video kupitia mitandao ya kijamii akisema, kujiunga na mfumo wa ushirikiano wa nchi za BRICS kutakuwa fursa nzuri ya maendeleo kwa Argentina, na kuifanya nchi hiyo kufungua ukurasa mpya.

Mohammad Jamshidi, naibu mkurugenzi wa ofisi ya rais wa Iran anayeshughulikia mambo ya siasa kupitia mitandao ya kijamii ameipongeza Iran akisema kwamba nchi hiyo kujiunga na mfumo wa nchi za BRICS ni hatua ya kihistoria na pia ni ushindi wa kimkakati wa sera ya kidiplomasia ya Iran.

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema kwenye mitandao ya kijamii kuwa, wakuu wa nchi za BRICS kuiunga mkono Ethiopia kujiunga na mfumo wa ushirikiano wa BRICS ni wakati mtukufu kwa Ethiopia. Nchi hiyo iko tayari kushirikiana na pande mbalimbali wakati wowote na kujenga utaratibu wa dunia ambao ni shirikishi na wenye ustawi.