TMA yatoa tahadhari ongezeko la mvua kubwa
2023-08-25 10:28:30| cri

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania (TMA), imesema kutokana na tahadhari ya uwepo wa El-Nino nchini humo, mvua kubwa zinatarajiwa kuonyesha katika msimu wa vuli mwezi Oktoba hadi Disemba mwaka huu.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Dk Ladislaus Chang'a, amesema mvua za vuli zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2023.

Tahadhari ya uwepo wa El-Nino inatokana na mabadiliko ya tabianchi ambapo hali ya joto la bahari la juu ya wastani, inaendelea kuongezeka katika eneo la kati la kitropiki la Bahari ya Pasifiki.

Kwa mujibu wa utabiri huo wa TMA, mvua za vuli zinatarajiwa kuwa juu ya wastani hadi wastani katika maeneo ya Pwani ya Kaskazini na ukanda wa Ziwa Victoria, pamoja maeneo ya machache ya Mashariki mwa Ziwa Victoria.