Xi Jinping akutana na Rais Samia wa Tanzania
2023-08-25 09:15:04| CRI

Rais Xi Jinping wa China amekutana na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wakati wa Mkutano wa 15 wa wakuu wa nchi za BRICS mjini Johannesburg.

Rais Xi amedokeza kuwa ziara yenye mafanikio ya Mheshimiwa Rais Samia nchini China mwezi Novemba mwaka jana ilikuja wakati muhimu katika uhusiano kati ya China na Tanzania. Makubaliano mbalimbali waliyofikia yanatekelezwa kikamilifu na kwa ufanisi. Ushirikiano kati ya China na Tanzania siku zote umekuwa mbele zaidi katika ushirikiano kati ya China na Afrika, na Reli ya TAZARA ni kumbukumbu nzuri ya watu wa nchi hizo mbili. Mwaka ujao China na Tanzania zinaadhimisha miaka 60 tangu zianzishe uhusiano wa kibalozi, hivyo China ina nia ya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kupitia fursa hii. Chini ya hali ya sasa ya kimataifa, kuimarisha ushirikiano kati ya China na Afrika ni jambo linalosaidia kulinda mshikamano na maslahi halali ya maendeleo ya nchi zinazoendelea.

Naye Rais Samia amefurahi kutembelea China mwaka jana na kuboresha uhusiano kati ya nchi hizo mbili hadi kuwa ushirikiano wa kimkakati na Rais Xi Jinping, akisema Tanzania na China zimedumisha mawasiliano ya karibu katika ngazi zote, na miradi ya ushirikiano inaendelea vizuri. Tanzania inathamini sana misaada na uungaji mkono wa China kwa maendeleo ya nchi zinazoendelea.

Ameongea kuwa Tanzania na nchi nyingine zinazoendelea zimenufaika sana na ujenzi wa pamoja wa pendekezo la "Ukanda Mmoja na Njia Moja" lililotolewa na Rais Xi Jinping. Tanzania inatarajia kuongeza zaidi kiwango cha maendeleo ya uhusiano kati ya Tanzania na China kupitia fursa ya maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi na China mwakani.