Kasi ya suluhisho la kisiasa nchini Sudan yaongezeka licha ya kuendelea kwa mapigano
2023-08-28 08:45:39| CRI

Mwenyekiti wa Baraza la Mpito la Utawala la Sudan, ambaye pia ni Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la nchi hiyo Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan ametembelea mji wa Port Sudan jana jumapili, na kuzusha hisia kwamba huenda hatua hiyo inalenga kutafuta suluhisho la kisiasa kwa mgogoro kati ya pande zinazopigana nchini humo.

Siku hiyohiyo, Kamanda wa Kikosi cha RSF Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo naye aliwasilisha pendekezo la kisiasa la suluhisho la kina la mgogoro unaoendelea nchini humo. Kupitia mtandao wa kijamii wa X, Jenerali Dagalo ametoa pendekezo la kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano, na pia kutoa vipengele vya suluhisho la kina la kisiasa kukabiliana na vyanzo vikuu vya vita nchini Sudan.

Pia amesisitiza umuhimu wa kuunda serikali ya kiraia ya kidemokrasia kwa msingi wa uchaguzi huru na wa usawa katika ngazi zote ili kuwawezesha raia wa Sudan kushiriki kikamilifu katika kuamua hatma yao kisiasa.