Naibu balozi wa kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Dai Bing ameitaka jumuiya ya kimatiafa kuisaidia Mali kukabiliana na changamoto baada ya Tume ya Ulinzi wa Amani ya Umoja wa Mataifa (MINUSMA) kuondoka nchini humo.
Balozi Dai amesema, hivi sasa mchakato wa amani nchini Mali upo katika kipindi muhimu, na MINUSMA inaondoka kutoka nchini humo hatua kwa hatua, na kuongeza kuwa, jumuiya ya kimataifa inatakiwa kuisaidia Mali kukabiliana na changamoto mbalimbali kutokana na hali ya jumla ya amani na utulivu nchini Mali na kanda nzima, na kuhimiza Umoja wa Mataifa kukuza ushirikiano na Mali chini ya hali mpya.
Akizungumzia hali ya usalama katika eneo la Sahel, Balozi Dai Bing amesema hivi sasa hali ya kisiasa katika nchi za eneo la Sahel ni ya wasiwasi, na makundi ya kigaidi na vikosi vyenye siasa kali vinatumia fursa hiyo kuleta machafuko na kutishia utulivu wa kikanda. Amesisitiza kuwa ni muhimu kuendelea kuunga mkono ushirikiano kati ya Afrika Magharibi na nchi za eneo la Sahel, kuimarisha mfumo wa ushirikiano na kulinda usalama wa pamoja baada ya kuondoka kwa MINUSMA.