China yaitaka jamii ya kimataifa kuunga mkono zaidi maendeleo ya vijana barani Afrika
2023-08-30 08:33:33| CRI

Naibu mwakilishi wa kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Dai Bing, amesema China imejikita katika kulinda amani na maendeleo ya Afrika, kuchukua hatua halisi kuunga mkono maendeleo ya vijana barani Afrika, na pia inapenda kushirikiana na jamii ya kimataifa kuunga mkono zaidi vijana wa bara hilo.

Balozi Dai amesema, hivi sasa baadhi ya nchi za Afrika zinakabiliwa na changamoto mbalimbali za vita, ugaidi na usalama wa chakula, na kundi lililo hatarini zaidi ni vijana. Amesema hivi karibuni China imezindua Pendekezo la Kuunga Mkono Utandawazi wa Viwanda Barani Afrika”, kutekeleza “Mpango wa China Kusaidia Ujenzi wa Mambo ya Kisasa ya Kilimo Barani Afrika”, na “Mpango wa Kuwaandaa kwa Pamoja Wataalamu wa China na Afrika.” Hatua hizo zinalingana na mahitaji ya sasa ya Afrika, na kusaidia maendeleo ya vijana barani humo kwa hatua halisi.

Pia amesema hatua za China za kuunga mkono zaidi vijana wa Afrika ni pamoja na kuonesha umuhimu wa vijana katika kuhimiza ufumbuzi wa kisiasa wa masuala yanayofuatiliwa, kuzuia mapambano ya silaha na kupunguza hatari za mapambano hayo kwa vijana, pamoja na kuhimiza amani kwa maendeleo.