Chama cha Upinzani nchini Zimbabwe Citizen’s Coalition For Change (CCC) kimepinga ushindi wa rais mteule wa nchi hiyo Emmerson Mnangagwa katika uchaguzi uliofanyika tarehe 23 na 24 mwezi huu, na kutaka uchaguzi huo urudiwe tena.
Naibu msemaji wa Chama hicho Gift Siziba amewaambia wanahabari mjini Harare, kuwa wanaamini kuwa uchaguzi huo hauonyeshi matakwa halisi ya Wazimbabwe, na kwamba kasoro mbalimbali zilijitokeza wakati wa uchaguzi.
Amesema kutokana na kasoro hizo, nchi hiyo inapaswa kujiandaa kwa uchaguzi mpya utakaosimamiwa na taasisi za kimataifa, ikiwemo Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika. Hata hivyo hakuweka wazi kama CCC itafuata sheria kupinga matokeo ya uchaguzi huo mahakamani.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe (ZEC) jumamosi, Mnangagwa amepata asilimia 52.6 ya kura zote zilizopigwa, huku mshindani wake mkuu Nelson Chamisa, kiongozi wa chama cha CCC akipata asilimia 44 ya kura zote.