Kila ifikapo tarehe 10 Septemba dunia inaadhimisha Siku ya kupinga na kuzuia matukio ya kujiua duniani. Kutokana na ukali na wingi wa matukio kama haya duniani hasa katika Afrika, Shirika la Afya Duniani WHO mwaka jana lilizindua kampeni mpya ili kutoa uelewa na kuchukua hatua kwa ajili ya kuzuia kujiua barani Afrika ambako kuna viwango vikubwa vya vifo vitokanavyo na kujiua. Kwa mujibu wa takwimu za shirika hilo karibu watu 11 katika kila watu 100,000 wanakufa kila mwaka kwa kujiua Afrika kikiwa ni kiwango kikubwa zaidi ya kiwango cha wastani cha kimataifa ambacho ni watu 9 kwa kila watu 100,000.
Hata hivyo cha kuhuzunisha zaidi ni kwamba idadi ya wanaume wanaojiua inaonekana kuwa kubwa zaidi kuliko wanawake. Kwa mujibu wa WHO, takribani watu milioni 4 huwaza na wengine hujaribu kujiua kila mwaka, lakini miongoni mwao ni takribani laki 8 ndio ambao huchukua uamuzi wa kujiua. Na kati ya watu watano wanaojiua duniani kote, wanaume ni wanne huku mwanamke akiwa mmoja, kwa upande wao wanasaikolojia wanaitaja sababu hiyo kuwa ni kutokana na asili ya mwanamke na mwanaume katika kuwasiliana pale wananapokuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ambapo mwanamke anaonekana kuwa mtu wa kuongea zaidi na kutoweka mambo moyoni huku mwanaume akionekana kuwa mtu wa kukaa kimya. Hivyo katika kipindi cha leo cha Ukumbi wa Wanawake tutaangalia sababu za matukio ya kujiua kwa watoto, vijana na wanawake.