Jeshi la Gabon latangaza mapinduzi ya kijeshi
2023-08-31 08:30:33| CRI

Kamanda mkuu wa Jeshi la Gabon Brice Oligui Nguema, ametangazwa kuwa kiongozi wa mpito wa Gabon jana usiku baada ya kutokea mapinduzi.

Awali, Tume ya Uchaguzi ya nchini humo ilitangaza kuwa rais Ali bongo ameshinda katika uchaguzi wa rais kwa muhula wa tatu, lakini hata hivyo, jeshi lilitangaza kupitia televisheni ya taifa kuwa matokeo hayo yamefutwa na kumzuia rais Bongo nyumbani kwake.

Msemaji wa Kamati ya Mpito na Urejeshaji wa Taasisi (CTRI) Ulrich Manfoumbi Manfoumbi amesema, viongozi wa Jeshi la Gabon wamekubaliana kwa kauli moja kumteua Nguema kuwa rais wa Kamati hiyo.

Jamii ya kimataifa imeeleza wasiwasi wake kuhusu mapinduzi hayo ya Gabon. Mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat ameeleza wasiwasi wake kuhusu hali ya nchini Gabon, na kupinga vikali mapinduzi kama njia ya kusuluhisha mgogoro wa uchaguzi nchini humo.