AU yalaani kuongezeka kwa mwenendo wa mabadiliko ya serikali kinyume na katiba barani Afrika
2023-09-01 08:34:25| CRI

Umoja wa Afrika (AU) umelaani vikali wimbi la mabadiliko ya serikali kinyume cha katiba barani Afrika, ambalo ni tofauti na taratibu za kawaida za Umoja huo.

Katika taarifa iliyotolewa na Baraza la Amani na Usalama la AU, baraza hilo limesisitiza haja ya dharura ya kuangalia upya ufanisi wa mwitikio wa Umoja huo kwenye changamoto hii.

Baraza limeelezea wasiwasi wake kutokana na kucheleweshwa kwa urejeshwaji wa haraka wa utaratibu wa kikatiba katika baadhi ya nchi wanachama wa Umoja huo, na kuzihimiza kuongeza juhudi ili kuhakikisha kazi zote za mpito zinatekelezwa kwa muda uliowekwa.

Taarifa hiyo imekuja siku moja baada ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Bw. Moussa Faki Mahamat kulaani mapinduzi yaliyotokea nchini Gabon, ambayo ni ya karibuni zaidi kati ya mfululizo wa mapinduzi katika bara hilo.