Marekani yavuruga usalama wa kijamii duniani kwa kuuzia nchi nyingine bunduki
2023-09-01 09:54:54| CRI

Katika miaka ya hivi majuzi, mauaji ya kufyatua risasi yamezidi kuwa ugonjwa sugu wa kijamii nchini Marekani. Wakati huo huo, Marekani inasafirisha maafa haya kwa nchi nyingine duniani kupitia kuziuzia bunduki, na kusababisha tishio kubwa kwa usalama wa kijamii duniani.

Shirika la Habari la Marekani Bloomberg hivi karibuni lilitoa ripoti ya uchunguzi, ikisema asilimia 37 ya bunduki zilizopatikana na kufuatiliwa katika matukio ya uhalifu katika nchi zisizo za bara la Amerika Kaskazini, zilisafirishwa kihalali kutoka Marekani, pamoja na bunduki zilizouzwa kwa njia haramu, kiwango hicho kinatisha zaidi.

Mwezi Oktoba mwaka jana, mauaji ya kikatili yalitokea katika shule ya chekechea kaskazini mashariki mwa Thailand. Muuaji huyu aliwaua watu 36, wakiwemo watoto zaidi ya 20 wenye umri wa miaka kati ya 2 na 5. Bastola iliyotumiwa na muuaji huyo iliuzwa nchini Thailand na Kampuni ya Sig Sauer, ambayo ni kampuni kubwa zaidi ya kuuza bunduki nje ya Marekani. Mauzo ya bunduki za Marekani kwa nchi za nje yameongezeka maradufu katika kipindi cha miaka sita iliyopita, na Thailand ni mojawapo ya nchi zilizoagiza zaidi bunduki hizo za Marekani. Takwimu zinaonyesha kuwa katika miaka hiyo sita, idadi ya matukio ya uhalifu yanayohusiana na bunduki nchini Thailand imeongezeka kwa asilimia 43.

Nchi jirani na Marekani zimeteseka zaidi kutokana na mauzo ya nje ya bunduki za Marekani. Kwa mfano, nchini Mexico, mwaka 2020, kati ya mauaji 24,600 yanayohusiana na bunduki, asilimia 70 na 90 ya bunduki hizo zilitoka nchini Marekani. Serikali ya Mexico ilikadiria kuwa hasara za kiuchumi kutokana na bunduki hizo zimekuwa dola bilioni 10 za Kimarekani. Wakati huohuo, idadi ya bunduki zinazoagizwa na Guatemala kutoka Marekani iliongezeka kutoka wastani wa takriban 3,600 kwa mwaka katika miaka ya 2010 hadi 20,000 mwaka 2022. Mauaji nchini humo ambayo yalikuwa yamepungua kwa miaka 11 mfululizo, yanaongezeka kila mwaka, na zaidi ya asilimia 80 ya mauaji hayo yanahusiana na bunduki.

Mauzo ya silaha ndogo zinazotengenezwa Marekani kwa nchi za nje yanatokana na kujipatia maslahi ya kibiashara. Kampuni ya Sig Sauer ya Marekai ilikuwa kampuni ndogo, lakini sasa imebadilika kuwa muuzaji mkubwa zaidi wa silaha ndogo kwa nchi za nje. Takiwmu zinaonesha kuwa imeuza zaidi ya bunduki 935,000 nje ya nchi katika miaka 10 iliyopita, na kupata faida kubwa mno, huku ikichochea uhalifu wa vurugu katika nchi nyingine.

Wizara ya Biashara ya Marekani pia imekuwa mhimizaji muhimu wa mauzo ya silaha ndogo kwa nchi za nje. Inazisaidia kampuni za nchi hiyo za bunduki kuvutia wanunuzi wa kigeni, kushiriki katika maonyesho husika ya kimataifa, na kutoa tovuti za mtandaoni ili kuzisaidia kupata wanunuzi wa kimataifa. Aidha, Marekani pia inajaribu kushawishi nchi nyingine kuruhusu raia wao kumiliki bunduki kihalali.

Marekani inajidai kama “mtetezi wa haki za binadamu duniani”, lakini kutokana na faida kidogo ya kibiashara, inauza ovyo silaha ndogo katika nchi za nje, ambazo zinatishia sana watu wa kawaida. Kwa mara nyingine tena imekuwa mharibifu wa haki za binadamu duniani.