Wanaharakati wa Afrika wataka kuhamia kwenye mifumo ya ufugaji inayostahimili mabadiliko ya tabia nchi
2023-09-01 08:36:50| CRI

Mabadiliko ya haraka kuelekea mifumo ya ufugaji iliyo rafiki kwa mazingira yatakuwa sehemu muhimu ya kuokoa jamii za wafugaji barani Afrika kutokana na majanga ya mabadiliko ya tabia nchi.

Hayo yamesemwa na wanaharakati Afrika siku chache kabla ya Mkutano wa Kilele wa Tabia Nchi wa Afrika utakaofanyika mjini Nairobi.

Mkurugenzi wa Afrika wa Shirika la Kulinda Wanyama Duniani (WAP) Bw. Tennyson Williams amesema taratibu zisizo endelevu za ufugaji barani Afrika zinazolenga kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya nyama, zimechochea utoaji wa hewa inayosababisha kuongezeka kwa joto duniani, na kutishia maisha ya wahamaji katika maeneo kame.

Bw. Williams amesema mifugo inahusishwa na takriban asilimia 34 ya uzalishaji wa hewa chafu, na hivyo kuhimiza uharaka wa kurejesha tena ufugaji usiosababisha uchafuzi kwa kutumia mbinu za nyumbani na marekebisho ya sera.