Mfumo wa BRICS+ wapongezwa na nchi za Afrika
2023-09-01 09:57:04| CRI

Mkutano wa 15 wa viongozi wa nchi za BRICS unafanyika nchini Afrika Kusini, ambapo viongozi wanaohudhuria mkutano huo wanajadili kwa kina mada mbalimbali ikiwemo kuimarisha ushirikiano na kupanua mfumo wa BRICS kuwa BRICS+.

Afrika Kusini, ambayo ni nchi mwenyeji wa mkutano huo, imewaalika viongozi wa nchi zote za Afrika kushiriki katika mkutano huo. Kabla ya hapo, nchi nyingi za Afrika zikiwemo Misri, Ethiopia, Zimbabwe, Algeria, Nigeria, Sudan na Tunisia zimeeleza nia yao ya kujiunga na mfumo wa ushirikiano wa BRICS, na baadhi yao zimewasilisha maombi rasmi.

Katika miaka ya hivi karibuni, nchi za Afrika zimezidi kutoridhika na mfumo wa usimamizi wa mambo ya kimataifa unaodhibitiwa na nchi zilizoendelea za Magharibi, zikilalamikia zaidi mfumo wa kifedha wa kimataifa ulioanzishwa baada ya Vita ya Pili ya Dunia. Mamalalamiko yanatokana na kwamba, sheria za kimsingi za mfumo huo zimetungwa na nchi zilizoendelea kama vile Marekani na nchi za Ulaya, na zinapuuza sana maslahi ya nchi zinazoendelea. Takwimu zinaonesha kuwa, kati ya mikopo ya dola bilioni 650 zilizotolewa na IMF mwaka 2021, dola bilioni 160 zilikwenda kwa nchi za Umoja wa Ulaya, huku nchi za Afrika zikipata dola bilioni 34 tu. Kulingana na idadi ya watu, mtu kutoka nchi tajiri za Umoja wa Ulaya alipata fedha karibu mara 13 kuliko mtu wa nchi maskini za Afrika. Zaidi ya hayo, nchi za Afrika zinalazimika kubeba gharama za mkopo ambazo ni mara 4 hadi 8 zaidi kuliko nchi zilizoendelea. Matokeo ya hali hii ni kwamba nchi tajiri zinazidi kutajirika huku nchi masikini zikizidi kuwa masikini, na ni vigumu kwao kutimiza maendeleo endelevu.

Kwa miaka mingi, nchi za Afrika zimekuwa zikitamani kuwepo kwa mfumo wenye nguvu wa nchi zinazoendelea ili kukabiliana na makandamizi ya nchi za magharibi, na sasa, mfumo wa ushirikiano wa BRICS umeleta matumaini. Mfumo huo ulianza mwaka 2006, na nchi wanachama wake zilichukua asilimia 26.46 ya ardhi yote ya dunia na asilimia 41.93 ya idadi ya watu duniani. Mwaka 2021, jumla ya uchumi wa nchi tano za BRICS ilifikia takriban asilimia 25.24 ya jumla ya uchumi wa dunia, na kupita Kundi la Nchi 7 (G7) linaloongozwa na Marekani. Kiwango cha mchango wa nchi za BRICS katika ukuaji wa uchumi wa dunia umezidi asilimia 50 kwa miaka mingi mfululizo. Wakati huo huo, kutokana na maendeleo ya mfumo wa BRICS, mada ya kupanua mfumo huo imewekwa kwenye ajenda, na kujadiliwa kwa kina katika mkutano huo wa Afrika Kusini, na kuzipatia nchi za Afrika fursa ya kujiunga na mfumo huo.

BRICS+ imetoa njia mpya kwa Afrika, ambayo ni kwamba, kwa kushirikiana na nchi wanachama wa mfumo huo, ambazo zote pia ni nchi zinazoendelea, na kukabiliwa na changamoto sawa na zenye maoni mengi sawa kuhusu mambo ya kimataifa, zinaweza kupata misaada ya maendeleo na kuhimiza kuboresha usimamizi wa mambo ya kimataifa, ili kutimiza kihalisi maendeleo endelevu.