Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) limesema watoto barani Afrika ni kati ya kundi lililo hatarini zaidi kuathirika na mabadiliko ya tabianchi, wakati ni asilimia 2.4 ya fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zikilenga kundi hilo.
Katika ripoti yake “Muda wa Kuchukua Hatua: Kufuatilia Watoto wa Afrika katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi”, iliyotolewa kabla ya Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi unaoanza leo mjini Nairobi, Shirika hilo limesema watoto wamesahaulika katika fedha zinazotolewa ili kuwasaidia kufanya mabadiliko, kuishi na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Pia ripoti hiyo imesema, watoto katika nchi 48 kati ya 49 barani Afrika waliofanyiwa tathmini wamewekwa katika ngazi ya juu ya hatari ya kuathirika na mabadiliko ya tabianchi.