Tanzania yaandaa kongamano la mabadiliko ya mifumo ya chakula barani Afrika
2023-09-05 08:42:53| CRI

Zaidi ya wajumbe 4,000 kutoka zaidi ya nchi 70 wanakutana nchini Tanzania kwenye Kongamano la 13 la kila mwaka la Mifumo ya Chakula Afrika, kujadili mabadiliko ya mifumo ya chakula barani Afrika.

Taarifa iliyotolewa na waandaaji wa kongamano hilo imesema kongamano hilo linafanyika Septemba 5-8 likiwa na kauli mbiu ya "Rejesha, Unda upya, Chukua hatua: Suluhu za Afrika kwa Mabadiliko ya Mifumo ya Chakula," linawakutanisha viongozi, na wavumbuzi kutoka kote duniani kujadili sera, mafanikio na uvumbuzi katika mabadiliko ya mifumo ya kilimo na chakula.

Waziri wa Kilimo wa Tanzania Bw. Hussein Bashe amesema kongamano hilo ni hatua muhimu katika safari ya kuanzisha mageuzi ya mifumo jumuishi na endelevu ya chakula katika bara zima la Afrika.