Watoto milioni 1.85 wakimbia makwao kutokana na mabadiliko ya tabianchi eneo la Afrika kusini mwa Sahara mwaka 2022
2023-09-05 08:45:02| CRI

Shirika la hisani la Save the Children limesema, watoto zaidi ya milioni 1.85 kwenye eneo la Afrika kusini mwa Sahara wamelazimika kukimbia makwao kutokana na majanga ya asili yaliyosababishwa na mabadiliko ya tabianchi mwishoni mwa mwaka 2022, idadi ambayo imeongezeka karibu maradufu katika miaka iliyopita.

Ofisa habari wa shirika hilo eneo la Afrika Mashariki na Kusini Bibi Kijala Shako amesema anatumai kuwa viongozi wanaoshiriki katika Mkutano wa Kilele wa Afrika Kuhusu Tabianchi watatambua kuwa msukosuko wa tabianchi una athari kubwa hasi dhidi ya maisha ya watoto na hivyo wataitikia mahitaji na haki za watoto.

Kwa mujibu wa shirika hilo, idadi ya wakimbizi wapya wa ndani katika eneo la Afrika Kusini mwa Sahara mwaka 2022 kutokana na majanga ya asili imefikia milioni 7.4, ikiwa imeongezeka mara tatu kuliko milioni 2.6 ya mwaka 2021.