Serikali ya Nigeria yatoa wito kwa vyama vya wafanyakazi kusitisha mgomo wa nchi nzima
2023-09-05 14:40:55| cri

Serikali ya Nigeria imetoa wito kwa Chama cha Wafanyakazi nchini humo (NLC) kufikiria upya uamuzi wao wa kuendelea na mgomo na badala yake kuendelea na mazungumzo, ikiwa ni hatua ya kukwepa mgomo wa nchi nzima ulioitishwa na Chama hicho kutokana na kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta.

Chama hicho kimependekeza kuanza mgomo wa siku mbili wa nchi nzima hii leo kupinga hali ngumu ya maisha inayotokana na kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta, suala ambalo limekuwa tete na lenye mvutano mkubwa nchini humo.

Akizungumza katika mkutano na wanahabai mjini Abuja, Waziri wa Kazi na Ajira Simon Lalong amesema uamuzi wa kugoma utaharibu maendeleo yaliyopatikana katika njia ya kutimiza hatma nzuri kwa wafanyakazi na wananchi wa Nigeria.

Amesisitiza kuwa serikali inajitahidi kutekeleza sera zinazolenga kuzalisha ajira kwa wingi katika sekta zote za uchumi, na kuwataka waandaji wa mgomo huo kuweka umuhimu Zaidi kwenye majadiliano badala ya mgomo.