Serikali kubuni mkakati mpya wa kuwafidia wahanga wa mashambulizi ya wanyama pori
2023-09-06 14:08:59| cri

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania, Dunstan Kitandula amesema serikali sasa inaandaa mkakati wa dharura wa kushughulikia malalamiko ya wahanga wa mashambulizi ya wanyama pori na wanyama wanaorandaranda,.

Hayo ameyasema bungeni wakati akizungumzia mpango huo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Yustina Rahhi, aliyeitaka serikali kutoa msimamo kuhusu uwezekano wa kuanzisha mfuko maalum kwa ajili ya kuwalipa fidia wahanga wa mashambulizi ya wanyama pori.

Kanuni za sasa za wanyamapori zinaelekeza kwamba walionusurika katika shambulio la wanyamapori wanapaswa kupokea fidia ya 200,000/-, huku wale waliopoteza viungo vya mwili wanapaswa kupokea 500,000/- na 1m/- kwa waliofariki.

Hata hivyo, naibu waziri huyo alisema serikali hailipi fidia kwa kupoteza maisha au majeraha yanayosababishwa na wanyama hatari wa porini. Inalipa tu faraja kwa wahanga waliopoteza maisha au kuumia.